Mwanamuziki Mkongwe, Papa Wemba amefariki baada ya kuanguka ghafla jukwaani wakati akitumbuiza na bendi yake mbele ya maelfu ya mashabiki wake, Jumapili (Aprili 24) nchini Ivory Coast.

Kipande cha video kilichochukuliwa kutoka kwenye tamasha hilo kinamuonesha mwanamuziki huyo ambaye jina lake halisi ni Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, akianguka ghafla akiwa katikati ya wachezaji na waimbaji wengine wa bendi yake.

Alikimbizwa haraka katika hospitali iliyokuwa jirani na eneo hilo lakini alitangazwa baada ya dakika chache kuwa amekata roho.

Waziri wa Utamaduni wa Congo amethibitisha kutokea kwa kifo cha Papa Wemba akikitaja kuwa ni pigo kwa kizazi kilichopo na tasnia ya muziki ya Congo kwa ujumla.

“Ni pigo kubwa kwa Congo na Afrika kwa Ujumla. Alikuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wote wa Congo,” alisema Waziri huyo wa Utamaduni wa Congo.

Chanzo cha kuanguka kwake jukwaani na kupelekea kifo chake bado hakujafahamika.

Papa Wemba alianza kung’ara kwenye tasnia ya Muziki Barani Afrika miaka ya 1970 akiwa na Bendi ya Zaiko Langalanga ambayo ilipata umaarufu mkubwa. Miaka ya 1980, Muziki wake ulikuwa mkubwa Zaidi baada ya kuhamia Jijini Paris na kupata nafasi ya kufanya ziara ya kuizunguka dunia akiwa na bendi yake.

Mwaka 2003 alipata majanga baada ya Serikali ya Ufaransa na Ubeligiji zilimpata na hatia ya kuwasaidia watu kupata Visa za kuingia nchini humo kwa kudanganya kuwa ni wanamuziki wa bendi yake. Hata hivyo, alikanusha vikali tuhuma hizo akieleza kuwa kuna watu walifanya hivyo kwa kutumia jina lake.

Dar24 tunatoa pole kwa wadau wote wa muziki Afrika na dunia nzima kwa ujumla. Apumzike kwa Amani. Amina!

Mabilioni ya Kikwete yaanza kuchunguzwa
Video Mpya: Lady Jay Dee - Ndindindi