Mashabiki wa Simba SC wanaendelea kutambia usajili unaofanywa na mabosi wao hadi sasa, huku utamu zaidi ni taarifa za winga Peter Banda kukubali kumpisha Luis Miquissone anayejiandaa kutua kambi ya timu hiyo iliyopo Uturuki katikati ya juma hili kurejesha burudani Msimbazi.

Banda ndiye aliyekuwa mrithi wa Luis mara alipouzwa Al Ahly ya Misri na kupewa jezi namba 1l aliyokuwa akiitumia winga huyo kutoka Msumbiji ambaye Simba SC inamrejesha klabuni kwa mkopo baada ya kumalizana na Wamisri, ingawa alishindwa kuonyesha makali na kutawaliwa na majeraha kila mara.

Habari za ndani ya Simba SC zinasema, Banda aliyekuwa amegoma kutolewa kwa mkopo akitaka avunjiwe mkataba uliosalia kikosini ili asepe jumla na kufanya mabosi wake kuumiza vichwa kabla ya kupata mwafaka na sasa Mmalawi anaondoka.

Sio Banda tu, bali hata winga Msenegal, Pape Ousmane Sakho naye dili la kutaka kuuzwa Ulaya limekaa vizuri na kutoa nafasi kwa Simba SC kuingiza majembe mawili ya kuhitimisha idadi ya nyotawa kigeni kwani kwa sasa tayari ina wachezaji 12.

Wakati Banda anampisha Luis ili kwenda sawa na kanuni ya usajili wa nyota wa kigeni ya Ligi Kuu, kwa upande wa Sakho mara dili lake likitiki itatoa nafasi ya kushushwa kipa mpya ambapo awali ilielezwa angeletwa Mbrazili Caique Luis da Santos kumsaidia Aishi Manula aliye majeruhi, kabla ya dili hilo kusitishwa.

Ipo hivi. Simba SC inapambana kukamilisha dili la Luis na kipa mpya, tayari kikosi kilikuwa na nyota 12 wa kigeni kwa mujibu wa sheria ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lakini kuibuka kwa ofa za Banda na Sakho kumeipa nguvu Simba kumalizana na Al Ahly ili kumrejesha Luis.

Chanzo cha kuaminika ndani ya Simba SC kimeeleza, klabu hiyo imepokea ofa ya Banda na ipo tayari kumruhusu kuondoka na imefanya mazungumzo naye kumtoa kwa mkopo au kumalizana naye jumla ili iweze kusajili nyota wapya wawili wa kigeni wa mwisho.

Thomas Tuchel amuengua kiaina Sadio Mane
Frenkie de Jong kufanywa chambo FC Barcelona