Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Askari wa Jeshi la Polisi na Maafisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Geita, mwanzoni mwa wiki huu walikunjana mashati wakimgombea shahidi aliyefikishwa mahakamani.

Taarifa kutoka mkoani humo zimeeleza kuwa shahidi huyo aliyetajwa kwa jina la Paulo Sitephano alifikishwa mahakamani na maafisa wa Takukuru Wilayani Bukombe mkoani humo kwa lengo la kutoa ushahidi, lakini alipofika aliwekwa chini ya ulinzi na kufungwa pingu na polisi kwa madai kuwa alikuwa anatafutwa kwa muda mrefu.

Kitendo hicho kilipelekea Kamanda wa Takukuru wilayani Bukombe kuwaomba polisi wamuachie shahidi wao atoe ushahidi kwanza ndipo mengine yaendelee, ombi lililokubaliwa na polisi.

Hata hivyo, baada ya kumaliza kutoa ushahidi, kulizuka varangati baada ya maafisa wa Takukuru kutaka kuondoka na shahidi wao kwa kutumia gari lao huku polisi wakilazimisha kumtia nguvuni.

Maafisa hao walirushiana maneno na kuanza kukabana mashati kila mmoja akidai kuwa na haki katika hilo. Lakini askari polisi waliongeza nguvu kwa kuita gari la doria lililofika na askari wa ziada na kufanikiwa kumchukua mtuhumiwa huyo.

Mashuhuda wa tukio hilo wameeleza kuwa baada ya mvutano huo, baadhi ya maafisa wa Takukuru walionekana wakiwa wamechaniwa mashati yao huku wakitoa lawama nzito kwa matumizi ya nguvu ya jeshi hilo.

Takukuru walitaka kwanza Polisi wakamilishe taratibu za kisheria ndipo wamkamate mtuhumiwa huyo ambaye kwao alikuwa ni shahidi na wana wajibu wa kumlinda.

Naye mwendesha Mashtaka wa Polisi mahakamani hapo, Elias Mgobela aliwalaumu maafisa wa Takukuru kwa kushindwa kuonesha ushirikiano na jeshi hilo.

“Kisheria, polisi wana haki ya kumkamata mtuhumiwa eneo lolote. Huyo shahidi wa Takukuru alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu na polisi. Ilikuwa ni jukumu la maofisa wa Takukuru kushirikiana na polisi kufanikisha kumkamata badala ya kuzuia,” alisema.

Maelezo ya Mgobela yalipingwa na Kamanda wa Takukuru wilayani humo, Chuzela Shija aliyeeleza kuwa  Jeshi la Polisi lilipaswa kuambatana na Takukuru hadi ofisini kwao ili wakamchukue mtuhumiwa wao.

“Isingewagharimu polisi kufuatana na maofisa wa Takukuru hadi ofisini, wakakamilisha taratibu za kiofisi na shahidi huyo, halafu wakamtia mbaroni. Ilihitajika busara ndogo sana kulimaliza suala hili, lakini bahati mbaya wenzetu walichagua kutumia ubabe na kutunishiana misuli,” alikaririwa.

Picha: Ne-Yo na Mkewe wapata baraka ya mtoto
Mahakama ya Mafisadi yaiva, Waziri aiweka wazi