Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Simon Sirro ameagiza kufanyika kwa operesheni ya mwezi mmoja kwa nchi nzima, ili kubaini mianya ya uhalifu na wahalifu.
IGP Sirro ametoa agizo hilo mkoani Dar es salaam wakati wa kikao kazi na watendaji wa jeshi la polisi mkoani humo, waliokutana kwa lengo la kufanya tathmini ya operesheni ya wiki moja iliyokuwa na lengo la kuwasaka wahalifu.
Amesema operesheni hiyo imekuwa na mafanikio makubwa, kwa kuwa wamefanikiwa kukamata silaha za moto pamoja na wahalifu waliokuwa wakijihusisha katika matukio mbalimbali ya kihalifu.
Mkuu huyo wa Jeshi la polisi nchini, pia amewaelekeza Makamanda wa Polisi kote nchini kufanya operesheni ya usalama barabarani dhidi ya magari yote yasiyokidhi vigezo vya kuwepo barabarani, ili kuwahakikishia usalama watumiaji wa vyombo vya moto.