Mahakama nchini Kenya, imewakuta na hatia ya mauaji Polisi watatu na mtu mmoja waliyoyatekeleza mwaka wa 2016 kwa kumuuwa wakili wa haki za binadamu, Willie Kimani na watu wengine wawili.
Mahakama hiyo iliyopo katika mji mkuu wa Kenya Nairobi, itatoa hukumu dhidi yao baadaye ambapo katika hukumu hiyo Mahakama ilimwachilia afisa wa nne wa mashtaka, kwa sababu ya ukosefu wa ushahidi.
Vifo vya wakili Kimani, Dereva teksi Joseph Muiruri na dereva wa pikipiki Josephat Mwenda yalisababisha maandamano ya amani na mgomo wa mawakili wa Kenya, wakitaka kusitishwa kwa mauaji ya Polisi ambayo baadhi ya watu wanasema yameenea.
Hata hivyo, maandamano hayo baadaye yaligeuka kuwa ya vurugu wakati madereva wa teksi za pikipiki walichoma moto kituo cha Polisi ambapo marehemu hao watatu wanaaminika walishikiliwa kabla ya kuuawa.
Taarifa ya Daktari iliyowasilishwa Mahakamani ilisema Tezi dume za Mwenda zilikuwa zimepondwa na fuvu lake lilikuwa limevunjika, na miili mingine miwili ilikuwa na majeraha ya kitu butu.
Polisi wa Kenya mara kadhaa wameshutumiwa kwa kuwaua washukiwa ambao hawana ushahidi nao, na mara nyingine wanashutumiwa kwa kuendesha vikundi vya mauaji, na kufanya kuwa ni miongoni mwa dhuluma za haki.
Wakili wa haki za binadamu, Willie Kimani alifanya kazi nchini Kenya kama mwanasheria wa Misheni ya Kimataifa ya Haki, kikundi cha kutetea haki chenye makao yake makuu nchini Marekani.