Katika kuhakikisha kuwa Haki za Binadamu zinazingatiwa na kuheshimiwa na kila mtu, Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, amewataka watetezi wa haki za binadamu nchini kutumia vyombo vya Sheria katika kutetea maslahi ya wananchi.

Ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya watetezi wa haki za binadamu yaliyofanyika Jijini Dar es salaam, amesema kuwa kulalamika peke yake hakusaidii kitu bali wanatakiwa kutumia vyombo vya sheria na mahakama kudai haki zao.

Amesema kuwa jamii imekuwa ikilalamika pembeni bila ya kuchukua hatua stahiki ambazo zitaweza kusaidia kutatua tatizo na kuweza kupata haki zao za msingi.

“Watu wamekuwa wakijitolea kufanya kazi ili kuhakikisha wanapata haki zao bila vikwazo vyovyote, niseme tu kwamba Serikali itafanya kazi kwa karibu nanyi ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao,”amesema Prof. Kabudi.

Hata hivyo, kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu, Bahame Nyanduga amesema kuwa mtu ni utu wa binadamu na kila mtu anahitaji kuheshimiwa ili amani iweze kutamalaki katika nchi.

Naye Balozi wa Umoja wa Ulaya, Roeland Van Geer, amesema kuwa kazi zinazofanywa na watetezi hao hapa nchini ni mhimu hivyo ameahidi kutoa ufadhili katika umoja wa watetezi hao.

Hatma ya Chadema 'EALA' kujulikana mwezi ujao
Video: CUF kwazidi kuchafuka, JPM atikisa watu 47,000