Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba SC Ismail Aden Rage, amewataka watanzania wote ikiwamo mashabiki wa klabu yake kuungana pamoja kuiombea Young Africans ili itinge Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2022/23.

Young Africans imetanguliza mguu mmoja hatua ya Fainali baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 katika mechi yake ya kwanza ya Nusu Fainali dhidi ya Marumo Gallants kutoka Afrika Kusini iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam juzi. Timu hizo zitarudiana juma lijalo huko Johannesburg, Afrika Kusini.

Rage, amesema ushindi walioupata Young Africans ni mzuri na unawafanya waende kucheza kwa kujilinda katika mchezo wa marudiano na hatimaye kusonga mbele katika michuano hiyo.

Rage amesema kwa sasa Young Africans inapeperusha bendera ya Tanzania, hivyo ni wajibu wa kila shabiki kuungana nao kwenye hatua waliyofikia.

“Kipindi cha kwanza Young Africans walitoa nafasi kwa wapinzani ambazo hawakuweza kuzitumia lakini kipindi cha pili walifanya vizuri na kushinda.

“Huu ni ushindi mzuri sana ambao Young Africans wameupata, wakienda Afrika Kusini, watacheza mpira wa kujilinda muda wote, wana nafasi kubwa ya kwenda hatua ya Fainali, hivyo nawatakia kila la kheri.

“Naomba Watanzania wote tuweke pembeni tofauti zetu na tuiombee Young Africans ifike Fainali kwa sababu inaiwakilisha Tanzania,” amesema Rage.

Yesu wa Kenya apandishwa kizimbani baada ya kujisalimisha
Mwanasiasa Benard Membe afariki Dunia