Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameeleza namna alivyokuwa akiumizwa na vipigo mfululizo ambavyo Taifa Stars imekuwa ikivipata.

Rais Kiwete ameyatoa ya moyoni juu ya mgojwa ‘Taifa Stars’ ambaye alikuwa amejitolea kwa hali na mali kumtoa ICU ya kufungwa na kuboronga, alipokuwa akilihutubia bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana mjini Dodoma.

Alisema licha ya jitihada za kuwagharamia makocha wazuri wa kigeni, amekuwa akishuhudia timu hiyo ikiboronga hata pale alipokuwa akiamua kuisapoti kwa kuingia uwanjani kuishangilia. Aliongeza kuwa ilimbidi aache kuingia uwanjani hapo baada ya kuambiwa kuwa kila anapoingia yeye uwanjani timu hiyo inafungwa.

Hata hivyo, licha ya kufanya uamuzi huo, Taifa Stars iliendelea kufanya madudu huku ikimnyima raha rais huyo aliyeiomba kumpa raha mapema alipoingia madarakani.

“Kila ukienda wanafungwa, mwisho ikafikia nikaona hawa wanataka kusema mimi ndiye nina nuksi, nikaacha kwenda,” alisema. “Lakini hata wakiamia Unguja…tatu,” alisema rais Kikwete kwa ucheshi, kauli ambayo iliwavunja mbavu wabunge na wageni waalikwa.

Lakini katika kuonesha kuwa mtoto akiuchafua mkono wa mzazi haukati akautupa bali huusafisha na kuendelea kumlea, rais Kikwete aliahidi kuhakikisha anakamilisha uanzishaji wa academy ya michezo kwa ajili ya kukuza vipaji vya watoto kabla hajaondoka madarakani.

Pia, aliwataka TFF kufanya kitu kuikomboa timu yetu ya Taifa ambayo inaonekana dhahiri kutofanya vizuri. “Lazima waliangalie hili na kulifanyia kazi kwa kuwa si sahihi.”

Okwi Akamilisha Alichokitilia Nia Denmark
Ibra Kadabra Adhamiria Kukutana Na Hasimu Wake Ujerumani