Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametengua uteuzi wa Makamanda watatu wa Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Waliotenguliwa ni Kamanda wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar Ali Abdallah Ali, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Kanali Ali Mtumweni Hamad na Mkuu wa Kikosi Maalum Cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM) Comodore Hassan Mussa Mzee.
Akitoa taarifa maalum kwa wananchi kupitia vyombo vya Habari Ikulu Jijini Zanzibar, Rais Mwinyi amesema kufuatia taarifa za uwepo wa wafanyakazi hewa katika Idara Maalum za SMZ, ambapo aliunda Kamati ya uchunguzi kwa kufanya uhakiki wa idadi ya wafanyakazi pamoja na viwango vya mishahara vinavyotolewa kea vikosi vyote.
Taarifa kwa umma juu ya ripoti ya Kamati ya Uhakiki iliyomfikia ilieleza kwamba kulikuwa na watumishi 381 waliokuwa wakilipwa mishahara bila ya kuwa katika utaratibu unaotakiwa ikiwa na maana kwamba hao ni watumishi hewa.
Amesema fedha zilikuwa zikipokelewa na kutumika katika kipindi chote hicho ambapo walikuwa katika vikosi hivyo na kueleza kwamba lililothibitika ni kwamba wakati Kamati imeanza kazi zake baadhi ya vikosi ikiwemo JKU walianza kutengeneza utaratibu wa kurasimisha uwepo wa wafanyakazi hewa.
Baadhi ya maafisa waliwahi kukamatwa katika nyumba ya mtu binafsi wakiwa wamevalia sare za Jeshi vijana na kuwapiga picha ili kuthibitisha kwamba wamo katika ajira rasmi.
Rais Mwinyi amesema kwamba imebainika fedha zilizotumika kwa upotevu ni kiasi cha Tsh. Bilioni mbili milioni mia mbili thelathini na tano, laki saba na ishirini na tano kutokana na fedha zilizokuwa zikitumika kwa wafanyakazi hao hewa.