Rais wa Kenya, William Ruto amemsifu kinara wa Upinzani Raila Odinga kwa kuikosoa serikali yake na kuifanya kuwajibika huku kukiwa na mjadala kuhusu maandamano makubwa yanayopangwa kufanyika kote nchini.
Ruto ameyasema hayo akiwa Nyandarua ambapo alimpongeza Waziri Mkuu huyo wa zamani na kambi yake kwa kushinikiza utawala wake kutekeleza ahadi alizotoa kwa Wakenya. Alishikilia kuwa ili walipa ushuru kuweza kupata thamani ya kodi zao kutoka kwa serikali yoyote, ni lazima kuwe na uwajibikaji.
Amesema, “Tunafanya kila tuwezalo kutekeleza na pia upinzani. Hatuna wasiwasi nao kufanya kile wanachofanya mradi tu kuongozwa na uzalendo, tunataka taasisi zetu za usimamizi zikiwemo za upinzani ziwezeshwe ili zihakikishe rasilimali za umma zinatumika ipasavyo. Ninaamini katika utawala ambao unawajibishwa kwa sababu ndio aina pekee ambayo italeta mageuzi.”
Aidha, ameongeza kuwa mgombeaji anayeibuka wa pili katika uchaguzi wa rais ana ufuasi mkubwa hivyo ni vyema awe na afisi yake ambapo wafuasi wake watawasilisha malalamishi yao na kusema “Marekebisho ya katiba yatakayopitishwa kuunda fomu ya kuongoza ukokotoaji wa mgao wa kijinsia kwa kuzingatia tu maseneta waliochaguliwa, wabunge na Wawakilishi wa Wanawake.”
Maagizo ya Ruto kwa wabunge wa Kenya Kwanza kuwasilisha mswada wa kubuni afisi ya upinzani, hata hivyo, yalikabiliwa na hisia mseto ambapo hapo awali alikashifiwa vikali na baadhi ya Wakenya wakimtuhumu kwa kujaribu kukiuka utawala wa katiba.