Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo, Juni 12, 2021 amezindua mtambo Cathlab unaotibu matatizo ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Mtambo huo mpya ulionunuliwa kwa Sh. Sh4.6 bilioni, unaoifanya Tanzania kuwa nchi pekee Afrika Mashariki inayoumiliki. Una uwezo wa kufanya uchunguzi na kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo, ukiwa umeunganishwa na mtambo wa Carto 3 System 3D&mapping electrophysiology System.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mtambo huo, Rais Samia aliwapongeza madaktari wa taasisi hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya, kwa kutumia mitambo ya kisasa iliyopo.

Alisema kuwa ingawa kuna mitambo, kazi kubwa inayofanywa na binadamu kwa kutumia mitambo hiyo ndiyo inayookoa maisha ya watanzania wengi.

Alimnukuu mwandishi mkongwe wa vitabu, raia wa Marekani, Bw. Elbert Hubbard aliyewahi kuandika, ‘mashine moja inaweza kufanya kazi za watu 50, lakini hakuna mashine inayoweza kufanya kazi ya mtu mmoja anayefanya kazi kwa bidi ya ziada/kwa umahiri.

“Jumla ya wagonjwa 5,959 wamefanyiwa upasuaji wa moyo kwa kutumia tundu dogo, ambapo ni watu 11 tu wamepoteza maisha baada ya upasuaji, sawa na asilimia 0.2,” alisema.

Alitoa mfano wa jinsi ambavyo ameoneshwa picha za wafanyakazi wa taasisi hiyo wakiwa wamechoka baada ya kutimiza majukumu yao, huku wakisubiri kazi iendelee muda mfupi ujao.

“Nakuahidi kwamba fanyeni kazi, changamoto nyingine mmenieleza huko ndani tutakwenda kuzifanyia kazi. Nimeoneshwa hadi picha madaktari wamefanya kazi usiku wamechoka, wamejibana kwenye kipembe wamelala. Sasa huyo aliyekwenda kuwapiga picha sijui ni nani, lakini walistahiki kulala. Mwingine yuko ngazini hoi, kalala hapohapo ngazini. Lakini amelala amepumzika anasubiri alfajiri mapema kuna oparesheni nyingine zinaendelea. Kwahiyo, hii ni kazi kubwa, hongereni sana,” alisema Rais Samia.

Rais Samia aliahidi kuwa kwakuwa mcheza kwao hutuzwa, Serikali ya Awamu ya Sita itaangalia maslahi ya madaktari na wafanyakazi wa taasisi hiyo.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Profesa Mohammed Janabi alisema pamoja na matibabu hayo, mtambo huo mpya pia utawezesha uwekaji wa vifaa visaidizi vya moyo, kizibua mishipa ya damu ya moyo .

“Tunaishukuru Serikali kuiwezesha JKCI, kufunga mtambo huu wa kisasa, ni teknolojia ya hali ya juu, tutaweza kuokoa maisha ya watu wengi wenye matatizo ya moyo ikiwemo mfumo wa umeme wa moyo kupitia mashine hii,” amesema Profesa Janabi.

Aidha, amesema mtambo huo utasaidia kuondoa adha ya watanzania wengi kusafiri kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupata matibabu ya moyo.

Serikali yapiga 'stop' vivuko viwili kufanya safari
Rais Samia azindua mtambo wa kutibu mfumo wa moyo