Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo Juni 12, 2021 amezindua mtambo mpya wa matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wenye thamani ya Sh4.6 bilioni, ambapo mitambo hiyo inaifanya Tanzania kuwa nchi pekee inayotoa matibabu ya hali ya juu ya kibingwa Afrika Mashariki na Kati.
Mtambo huo wenye uwezo wa kufanya uchunguzi na matibabu ya moyo uliounganishwa na mtambo wa Carto 3 System 3D&mapping electrophysiology System, una uwezo wa kufanya uchunguzi na kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohammed Janabi amesema kazi zitakazofanywa na mtambo mpya wa kisasa wa kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo na kuchunguza mishipa ya damu ya moyo, kuweka vifaa visaidizi vya moyo, kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba na kutibu mfumo wa umeme wa moyo.
Aidha mtambo huo wa kisasa zaidi ya Cathlab wenye uwezo mkubwa zaidi wa kuchunguza na kutibu tatizo la hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo, ulianza kufanya matibabu kwa mgonjwa wa kwanza Aprili 30, 2021.
“Tunaishukuru Serikali kuiwezesha JKCI, kufunga mtambo huu wa kisasa, ni teknolojia ya hali ya juu, tutaweza kuokoa maisha ya watu wengi wenye matatizo ya moyo ikiwemo mfumo wa umeme wa moyo kupitia mashine hii.” Amesema Profesa Janabi.
Amesema kwa kipindi kirefu wagonjwa wengi walikuwa wakienda kutibiwa nje ya nchi na baadhi yao walitibiwa nchini na kwamba mtu anaweza kuzaliwa na tatizo hilo au kulipata ukubwani kutokana na athari ya ugonjwa unaoweza kusababisha mfumo wa umeme wa moyo kubadili mapigo yake.