Waziri wa nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,Bunge na Uratibu George Simbachawene, amesema Rais Samia  Suluhu Hassan anatarajia kutangaza   Matokeo ya Mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi  ya Mwaka 2022 pamoja na muongozo wa matumizi ya matokeo hayo.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma ambapo amesema Oktoba 31,2022 historia itaandikwa katika uwanja wa Jamhuri Dodoma

Waziri Simbachawene amesema kuwa uzinduzi huo ni tukio muhimu katika historia ya maendeleo ya nchi ndio maana Serikali imeamua kuhakikisha kunakuwa na uwakilishi wa wananchi wa makundi yote ili waweze kushiriki katika tukio hili la kihistoria.

“Oktoba 31 ni siku maalum kwa taifa letu hivyo basi hatuna budi kuhakikisha kwa tuliopo Dodoma na mikoa ya jirani tunajitokeza kwa wingi uwanja wa Jamhuri na wale tutakaokuwa mbali tufuatilie uzinduzi huo kupitia vyombo vya habari ili tushiriki pamoja na Mheshimiwa Rais kujua tupo wangapi wakati atakapotangaza Matokeo hayo ya Mwanzo,”amesema

Simbachawene amesema kuwa katika zoezi hilo wegeni wengine ni pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Marais hao wastaafu watatunukiwa tuzo maalum kwa kufanikisha Sensa katika vipindi vya uongozi.

“Sensa ya Watu na Makazi hufanyika mara moja kila baada ya miaka kumi na matokeo yake ndio yanayotumika katika kufanya maamuzi yote muhimu yanayohusu maendeleo ya nchi kwa kipindi cha miaka kumi hadi Sensa nyingine,hivyo

Amewataja baadhi ya Wageni watakaoshiriki katika Uzinduzi huo kuwa ni viongozi wa Serikali wakiwemo mawaziri na manaibu waziri, Makatibu wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu wa Serikali zetu zote mbili, Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Zanzibar, viongozi wa vyama vya Siasa na wawakilishi wa makundi mbalimbali katika jamii.

“Wageni wengine mashuhuri ni pamoja na Waheshimiwa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao humu nchini, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa yakiwemo ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika na Wadau wengine wa Maendeleo,”amefafanua Simbachawene.

Aidha amesema katika sherehe hizo, mbali ya kuzindua Matokeo ya Mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Rais Samia atazindua pia Mwongozo Maalum wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ambao lengo lake kuu ni kuhakikisha matokeo ya Sensa yanatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Matokeo haya ni muhimu sana kwa makundi yote katika jamii, wafanyabiashara, wakulima, wafugaji na hasa kwa Serikali yetu inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwani Serikali itaweza kupanga mipango yake kwa ajili ya maendeleo ya wananchi kulingana na idadi, mahitaji na mazingira wanamoishi,”

Ametoa  wito kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma na Mikoa jirani kujitokeza kushuhudia uzinduzi huo na wahakikishe wanafika majira ya saa 12 kamaili asubuhi.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Hamza  Hassan Juma amesema watakuwa na ujumbe wa  watu zaidi ya 150 watakaoshiriki siku hiyo .

Juma amesema sensa ya mwaka huu ilifanikiwa kwa kiwango cha juu kwa sababu ya kuungwa mkono na viongozi wa kisiasa na kidini .

Mashindano ya 12 duniani urembo,utanashati kwa viziwi kufanyika Tanzania
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Octoba 29, 2022