Rais wa zamani wa Iran ambaye pia alikuwa kiongozi wa ngazi ya juu wa kidini nchini humo, Akbar Hashemi Rafsanjani alifariki dunia jana akiwa na umri wa miaka 82.
Rafsanjani ambaye aliliongoza taifa hilo tangu mwaka 1989 hadi 1997, alifariki dunia kutokana kushambuliwa na mshtuko wa moyo.
Taarifa rasmi zilizotolewa na Serikali ya Iran kuhusu kifo cha mwanasiasa huyo zilieleza kuwa baada ya kukabiliwa na mshtuko wa moyo, alikimbizwa katika Hospitali ya Shohadaa jijini Tehran lakini madaktari walishindwa kuokoa maisha yake.
Serikali ya nchi hiyo imeitangaza siku tatu za maombolezo, na kwamba ya Jumanne wiki hii kiongozi huyo atazikwa kwa heshima zote jijini Tehran.
Rafsanjani anakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika mapinduzi ya mwaka 1979 ya nchi hiyo na baadae kuwa mwanasiasa imara.
Kiongozi wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei ambaye alikuwa mpinzani wa Rafsanjani ametoa salamu zake za rambirambi na kueleza kuwa alikuwa mpambanaji. Alisema tofauti zao za kimtazamo haziwezi kuwa sababu ya kuvunja urafiki na udugu wao.