Rais wa zamani wa Pakistani, Jenerali Pervez Musharraf (79) amefariki dunia mjini Dubai baada ya kuugua kwa muda mrefu katika Hospitali ya Marekani ya Dubai, huku Waziri mkuu wa nchi hiyo, Shehbaz Sharif akitoa salamu za pole kwa familia ya kiongozi huyo.
Mwenyekiti wa Baraza la Seneti la Pakistan, Muhammad Sadiq Sanjrani wa chama cha Tehreek-e-Insaf, kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Imran Khan ambaye aliondolewa madarakani kwa kura ya kutokuwa na imani naye mwaka jana, kilisema “Dua zetu na rambirambi ziende kwa familia yake na tunashiriki huzuni yao.”
Kiongozi huyo wa zamani, ambaye alikuwa akiishi uhamishoni huko Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu tangu 2016, alichukua madaraka kutoka kwa Waziri Mkuu wa zamani Nawaz Sharif kaka mkubwa wa Shehbaz Sharif katika mapinduzi ya kijeshi mnamo 1999 na kujiteua kuwa rais mnamo 2001 ambapo aliendelea kuiongoza Pakistan kama rais hadi 2008
Musharraf alikua mshirika mkuu wa Marekani kufuatia mashambulizi ya kigaidi ya 9/11, na alijaribu kuwa mtu muhimu sana katika kupambana na itikadi kali za Kiislamu, lakini muda wake madarakani uligubikwa na utata na alishutumiwa kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na ukandamizaji.
Muhula wake, ulihitimishwa na majaribio mawili ya mauaji yaliyofeli mwaka 2003. Mnamo Novemba 2007, alitangaza hali ya hatari, akasimamisha katiba ya Pakistan, akachukua nafasi ya jaji mkuu na kuzima vituo huru vya televisheni.
Musharraf alisema alifanya hivyo ili kuleta utulivu nchini humo na kupambana na kuongezeka kwa itikadi kali za Kiislamu. Hatua hiyo iliibua shutuma kali kutoka kwa Marekani na watetezi wa demokrasia na wapakistani walitaka waziwazi kuondolewa kwake.
Chini ya shinikizo kutoka Magharibi, Musharraf baadaye aliondoa hali ya hatari na kuitisha uchaguzi, uliofanyika Februari 2008, ambapo chama chake kilifanya vibaya na alijiuzulu mnamo Agosti 2008 baada ya muungano unaotawala kuanza kuchukua hatua za kumshtaki.
Musharraf alienda uhamishoni lakini akarejea Pakistan mwaka 2013 kwa lengo la kugombea katika uchaguzi wa kitaifa wa nchi hiyo. Badala yake, mipango yake ilivurugika alipojiingiza katika mtandao wa kesi za mahakama zinazohusiana na muda wake madarakani.
Mnamo 2019, alihukumiwa kifo bila kuwepo kwa uhaini mkubwa na hukumu hiyo ilibatilishwa baadaye na alikuwa akiishi Dubai tangu Machi 2016, wakati Mahakama ya Juu ya Pakistan ilipoondoa marufuku ya kusafiri, na kumruhusu kuondoka nchini kutafuta matibabu huko.