Rais wa Afrika kusini, Cyril Ramaphosa amesema kuwa Ujerumani ni mshirika muhimu wa kiuchumi wa nchi hiyo ambapo ameonyesha matumaini juu ya ushirikiano huo kupanua fursa za uwekezaji wa Ujerumani katika nchi yake.
Ramaphosa ameyasema hayo jijini Cape Town wakati rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier akimaliza ziara yake ya siku tatu nchini humo.
Ramaphosa amesema kuwa Ujerumani ni mshirika mkubwa wa tatu duniani wa kibiashara wa Afrika Kusini na ni mmoja kati ya wawekezaji wakubwa wa kigeni katika nchi hiyo. amesema kuwa zaidi ya makampuni 600 ya Ujerumani yanafanyakazi nchini Afrika Kusini, ambapo yameweza kutengeneza nafasi zaidi ya laki moja za kazi.
“Kama ilivyoonekana katika mazungumzo yetu na viongozi wa makampuni ya Ujerumani mjini Berlin mwezi uliopita, Afrika Kusini inaonekana kuwa sehemu muhimu ya uwekezaji, na kuna hamasa kubwa kwa makampuni ya Ujerumani kupanua uwapo wao hapa.”amesema Ramaphosa
Hata hivyo, Ujerumani na Afrika Kusini zitakuwa wanachama ambao si wa kudumu katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2019 na 2020 na rais, Cyril Ramaphosa amesema wamekubaliana kwamba nchi zao zitafanyakazi kwa pamoja kuhimiza amani ya dunia nausalama pamoja na kuimarisha mfumo wa ushirikiano wa pamoja.