Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete amemuomba Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage amfikishie Rais John Pombe Magufuli (JPM) salamu za wananchi wa jimbo hilo kuwa wanahitaji maji.
Ametoa ombi hilo wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika ujenzi wa Kiwanda cha Vigae Twayford kinachojengwa na raia wa China katika kijiji cha Pingo wilayani Kibaha.
Amesema kuwa kiwanda hakiwezi kuwa bora bila watu lakini wanashida kubwa ya maji ambayo inaweza ikasababisha kudumaa kwa maendeleo kijijini hapo.
“Chalinze ni eneo zuri kwa kiwanda cha aina yeyote, bado kuna tatizo kubwa la upatikanaji wa maji, Serikali ya awammu ya tatu iliahidi kumalizia na baadaye CCM, mwaka 2003 tulishuhudia mradi mkubwa wa maji ukijengwa wa Wami Chalinze chini ya ufadhili wa China, lakini bado leo hatuna maji,”amesema Ridhiwan.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage amewataka wananchi katika mpango wa upitishaji maji kutoka Mto Ruvu wasiweke kikwazo cha kutoa eneo la kupitisha maji kwa kudai fidia.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo amesema kuwa halmashauri zote zinaendelea kutenga maeneo ya viwanda kwaajili ya uwekezaji.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho, Jack Feng amesema kuwa Kampuni hiyo itawekeza Dola milioni 56 za Marekani ambazo ni sawa na Sh. 120 bilioni za kitanzania katika ujenzi wa kiwanda, ununuzi wa mitambo na vifaa mbalimbali.