Watumishi sita wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro wamefukuzwa kazi kwa kusababisha halmashauri hiyo kupata hati yenye mashaka katika kipindi kilichoishia Juni 30 mwaka 2020.
Akitoa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mkurugenzi wa halmashauri ya Siha, Ndaki Mhuli amesema sababu zilizochangia halmashauri hiyo kupata hati yenye mashaka ni ukusanyaji maduhuli ya shilingi milioni 112.5 bila kupelekwa benki na kufanyika kwa matumizi ya shilingi milioni 101.5 bila kuwa na viambatanisho.
Ametaja sababu nyingine kuwa ni kutoonekana kwa hati za malipo zenye thamani ya shilingi milioni 59.2 wakati wa ukaguzi pamoja na kutoonekana kwa viambatanisho vyenye thamani ya shilingi milioni 10 kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa kupitia kwenye akaunti ya kijiji cha Ngarenairobi.
Ndaki amesema mbali na watumishi hao sita kufukuzwa kazi, pia wapo watumishi wanne wanaokatwa fedha kwenye mishahara yao, na mmoja akipunguziwa asilimia 15 ya mshahara wake kwa muda wa miaka mitatu.
Aidha, amefafanua kuwa watumishi hao waliofukuzwa kazi ni kutoka Idara ya fedha na Idara ya manunuzi.