Watu 23 wamepoteza maisha baada ya lori la mafuta kupinduka na kushika moto kwenye barabara yenye msongamano katika Jimbo la Kogi, Nigeria.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Aljazeera, dereva wa lori hilo alishindwa kulidhibiti, likagonga magari matano, bajaji tatu na pikipiki mbili katika barabara ya Lokoja-Abuja, Jumatano wiki hii.
Taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari vya nchini humo imeeleza kuwa kati ya magari matano yaliyohusika kwenye ajali hiyo, watu wa familia moja walipoteza maisha baada ya gari walilokuwa wamepanda kupinduka na kuteketea kwa moto.
Kamanda wa Idara ya Usalama Barabarani katika Jimbo la Kogi, Idris Fika Ali amethibitisha idadi hiyo ya vifo. Ameeleza kuwa mtoto mmoja amenusurika kufa ingawa amepata majeraha makubwa.
Ajali hiyo imesababisha vifo vya watu waliokuwa kwenye magari 10 yaliyoathirika na ajali hiyo, kwa mujibu wa Ali.
Rais Muhammadu Buhari ametuma salamu za rambirambi na kueleza jinsi alivyoguswa na tukio hilo.
“Kamisheni ya Usalama Barabarani imethibitisha kuwa watu 23 wamefariki dunia, hii inawakilisha tukio lingine baya na la ghafla katikati ya majanga mengine ambayo yanaikumba nchi yetu,” amesema Rais Buhari.
Ameongezaa kuwa mfululizo wa majanga haya unampa wasiwasi kwa sababu yanasababisha vifo visivyo vya lazima, na mengine yanazuilika.