Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) limesema kuwa lina amini Rais wa Urusi, Vladimir Putin amehusika katika kufanya kampeni za siri za kumchafua na kumpunguzia nguvu mgombea urais kwa tiketi ya Democratic, Joe Biden ili Rais Donald Trump ashinde uchaguzi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na The Washington Post kwa kukariri chanzo cha habari kilichoona ripoti ya CIA, imeeleza kuwa Shirika hilo linaamini kuwa Putin amemtumia mbunge wa Ukraine, Andriy Derkach.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa Derkach alitumia njia mbalimbali kusambaza taarifa za kumuangusha Biden chini Marekani, ikiwa ni pamoja na kutumia vyombo vya habari na watu ambao wako karibu na Rais Trump.

The Washington Post limeeleza kuwa aya ya kwanza ya ripoti hiyo inasomeka, “tunatambua kuwa Rais Vladimir Putin na viongozi wengine waandamizi wa Urusi wanafahamu na huenda wanahusika moja kwa moja kusaidia shughuli zinazolenga kumharibia umaarufu na heshima makamu wa rais wa zamani wa Marekani, Joe Biden na kumpunguza nguvu mbele ya umma kuelekea uchaguzi mkuu wa Novemba, 2020.”

Imeeleza kuwa Derkach ana uhusiano wa karibu na Rudy Giuliani ambaye ni mwanasheria binafsi wa Rais Trump.

Pia, Derkach ametajwa na mkurugenzi wa ujasusi wa Marekani pamoja na Idara ya Hazina kuwa ni wakala wa Urusi.

Hata hivyo, Derkach ameendelea kukana taarifa hizo zinazotolewa na vyombo tofauti vya Marekani.

Taarifa hiyo meibua joto kwenye siasa za Marekani katika kipindi hiki cha kampeni za urais wa Marekani, kukiwa pia na taarifa za hivi karibuni za CIA zilithibitisha kuwa Rais Putin wa Urusi aliingilia mchakato wa uchaguzi wa mwaka 2016 na kumsaidia Trump kumshinda Hillary Clinton.

Wakati huohuo, chama cha Republican kimetangaza nia ya kutoa ripoti maalum kwenye Bunge la Seneti ya uchunguzi dhidi ya Biden na mwanaye wa kiume kuhusu shughuli zenye utata walizokuwa wanazifanya nchini Ukraine.

TRA yaja na mikakati hii
KMC FC kucheza na Kagera Sugar kesho Kaitaba

Comments

comments