Hatimae gwiji wa soka nchini Brazil Ronaldo Luís Nazário de Lima, ameafiki kununua asilimi 51 ya hisa za klabu ya Real Valladolid inayoshiriki ligi kuu ya soka Hispania (La Liga).
Ronaldo ameafiki kununua asilimia 51 za klabu hiyo, ambazo zitamgharimu kiasi cha Pauni milioni 27, baada ya kuzungumza kwa kina na rais wa sasa wa Real Valladolid, Carlos Suarez.
Katika mazungumzo ya wawili hao, Ronaldo amemtaka Suarez kuendelea kuwa kiongozi wa klabu hiyo hadi hapo atakapopata uongozi madhuhuti ambao anaamini utatosha kuiendesha klabu hiyo, ambayo ataimiliki kwa asilimia kubwa ya hisa.
Hatua ya gwji huyo mwenye umri wa miaka 41 kufikia maamuzi ya kuinunua klabu hiyo inayoshiriki ligi kuu msimu huu, ikitokea ligi daraja la kwanza Hispania, yatamuwezesha kurejea rasmi katika shughuli za soka nchini humo, baada ya kuondoka Real Madrid mwaka 2007.
Ronaldo pia aliwahi kuitumikia FC Barcelona kuanzia mwaka 1996–1997 na kisha alitimkia Italia kujiunga na Inter Milan (1997–2002), kabla hajarejea tena Hispania akisajiliwa na Real Madrid.
Ronaldo anaendelea kukumbukwa katika medani ya soka duniani, kufuatia kuwa mfungaji bora wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2002, sambamba na kuiwezesha timu ya taifa ya Brazil kutwaa ubingwa wa fainali hizo kwa kuifunga Ujerumani mabao mawili kwa sifuri.
Pia aliwahi kutangazwa kuwa mchezaji bora wa dunia wa FIFA mwaka 1996, 1997 na 2002.