Rais wa Kenya, William Ruto ametetea mapendekezo yake aliyoyatoa Bungeni ya kutaka mabadiliko ya katiba ili kurejeshwa kwa ofisi ya kiongozi wa upinzani, na kukanusha madai kuwa anafanya hivyo ili kumpa kazi mpinzani wake mkuu, Raila Odinga.
Ruto, ameyasema hayo wakati akifanya mahojiano na Waandhishi wa Habari na kuongeza kuwa hata yeye (Raila Odinga), hadhani kama anaitaka hiyo kazi hivyo watu waache kutafuta majibu ambayo si sahihi.
“Wale wote wanaodhani hivyo waelewe mimi simtafutii mtu kazi, nimeona kiongozi wa upinzani (Raila Odinga), akisema yeye hataki hiyo kazi, Nani alisema mimi natafutia mtu kazi?” Alifafanua na kuuliza Rais Ruto.
Katika hatua nyingine, Rais Ruto ametetea uamuzi wa serikali yake kuagiza mahindi yaliyozalishwa Kisayansi maarufu kama GMO, ili kusaidia kupambana na ongezeko la kupanda kwa gharama ya maisha na kukanusha ripoti kuwa ni hatari kwa matumizi.
Amesema,“Mimi kama kiongozi wa nchi siwezi kuhatarisha masiha ya watu walionichagua, umesikia mtu amemea pembe huko Afrika kusini kwa sababu amekula GMO.”