Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania imesema kuwa kiingereza kitaendelea kuwa lugha ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi ya elimu ya Sekondari, Vyuo vya kati na Vyuo vikuu hapa nchini.
Akizungumza Bungeni Jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako amesema kiingereza kitaendelea kutumika kwasababu ya umuhimu wake kitaifa, kikanda na kimataifa kwa mawasiliano na biashara ili kuwajengea wanafunzi ufahamu na umahiri wa lugha hiyo.
Amesema suala la matumizi ya lugha ya kufundishia na kujifunzia ni la kisheria kama ambavyo sheria ya elimu sura 353 inavyoeleza, sheria hiyo inabainisha matumizi ya lugha mbili za kufundishia na kujifunzia ambazo ni kiswahili na kiingereza.
Kwa sasa lugha ya kiswahili inatumika kufundishia katika ngazi ya elimu ya awali na elimu ya msingi, vyuo vya ualimu ngazi ya cheti na vyuo vya ufundi stadi hapa nchini.