Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally amemkingia kifua Kiungo kutoka nchini Burkina Fasso Ismail Sawadogo, kufuatia kuangushiwa lawama na baadhi ya mashabiki baada ya mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Simba SC ilipoteza 3-0 dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es saalaam, ambapo Sawadogo analalamikiwa kuwa tatizo lililozalisha bao la kwanza.
Ahmed Ally amesema kiungo huyo aliyesajiliwa wakati wa Dirisha Dogo msimu huu, ana kiwango bora na muda si mrefu atawafunga midomo wanaomtupia lawama.
“Ismael Sawadogo ni moja ya wachezaji wenye kiwango cha kipekee sana, muda utazungumza kwa sasa ni mapema mno kumuhukumu kwa sababu alikuwa nje kwa muda mrefu ila kwa sasa ameanza kurejea taratibu uwanjani.”
“Kwenye football ukishakaa nje kwa miezi kadhaa inaanza kukutoa kwenye shape lakini kama una unajua (If you know, you know), Sawadogo anajua mpira na muda utafika miguu yake itazungumza.”
“Sawadogo si mchezaji wa kumzungumzia sana, kumpamba sana mguu wake wa kushoto utatuambia yeye ni nani na amekuja Tanzania kufanya nini.” amesema Ahmed Ally
Kabla ya kusajiliwa Simba SC Sawadogo aliwahi kuzitumikia klabu za Difaâ El Jadida (Morocco), Enppi SC (Misri), Al-Arabi SC (Sudan), Al Mabarra Club (Lebanon), US Ouagadougou, Salitas, RC Kadiogo na AS Douanes (Burkina Faso).