Kaimu Afisa Habari wa Azam FC Hasheem Ibwe amewatumia salamu Simba SC kwa kusema wajiandae kupambana kwenye mchezo wa kesho Jumanne (Februari 21), kwani hali huenda ikaendelea kuwa ngumu upande wao.

Ibwe amefikisha salamu hizo, alipozungumza na Waandishi wa Habari leo Jumatatu (Februari 20), katika Mkutano maalum uliofanyika Ofisi Kuu za Benki ya NBC jijini Dar es salaam.

Hata hivyo amesema wanatambua mchezo utakua mgumu kutokana na mazingira waliyokutana nayo Simba SC kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Raja Casablanca na Horoya AC.

“Tunajua Mchezo dhidi ya Simba utakuwa mgumu kwa sababu wanatafuta pa kufufukia baada ya kupoteza michezo miwili mfululizo”

“Lakini Simba hawatakuja kirahisi na sisi hatutawapokea kirahisi, tutaingia kwa displini ili kuhakikisha tunaondoka na alama tatu”

“Tunawaomba mashabiki mje kwa wingi kutupa sapoti, hata wale mashabiki wa MKOPO mje mnakaribishwa” amesema Ibwe

Kesho Jumanne (Februari 21) Simba SC itakuwa nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, ikiwa na jukumu la kulipa kisasi cha kupoteza dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Duru la Kwanza la Ligi Kuu, ambapo bao lililofungwa na Mshambuliaji Prince Dube lilitosha kuizamisha miamba hiyo ya Msimbazi.

Simba SC inakweda kwenye mchezo huo ikiwa imejikusanyia alama 53 zinazoiweka nafasi ya pili katika msimamo, huku wapinzani wao kutoka Chamazi wakishika nafasi ya nne kwa kumiliki alama 43.

Rais Dkt. Mwinyi afungua ubalozi mdogo UAE
Suluhu mifumo usambazaji maji safi, usafi wa mazingira yaja