Tasnia ya Habari ni Mhimili muhimu unaofanyakazi ya kupokea taarifa kutoka vyanzo mbalimbali na kuzipitia kisha kuzifikisha kwa wananchi kwa lengo la kuhabarisha umma.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Maadili Jaji Sivangilwa Mwangesi katika mkutano wa Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa umma na Wahariri wa vyombo vya habari nchini kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali yenye kujenga afya katika uwasilishaji wa taarifa kutoka kwenye mamlaka hiyo kwenda kwa jamii.
“Tunaamini kuwa ninyi mkielewa vizuri mtaisadia jamii kuielewa vizuri Mamlaka ya taasisi yetu, na mtaitendea haki taaluma yenu na mtazichakata vizuri habari zozote ambazo zitawafikia katika madawati yenu kuhusiana na viongozi wa umma na ukiukwaji wa mahadili kwa viongozi wa umma. Mtazihoji na kuzidadisi taarifa hizo, kuzipembua na kuziangatia matakwa na mazingatio ya Sheria” amesema Jaji Mwangesi.
“Katika mkutano wetu huu wa leo malengo yetu ni kuongeza ushirikiano kati yetu na nyinyi Wahariri wa vyombo habari ili kutoa taarifa sahihi, kubadilishana mawazo ,kupeana ushuri wenye afya ili kujenga kitu kizuri kutoka kwetu kwenda kwa umma”
Ameongeza kuwa “tunaamini kuwa taarifa zetu zikiwa kamilifu, kupitia kwenu, majukumu na mamlaka yetu kwa mujibu wa ibara ya 132 ya mujibu wa Katiba yetu ya Tanzania wa mwaka 77, na Sheria ya Maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995, ambazo ni Sheria tunazozifanyia majukumu yake zitaeleweka vizuri kwa wadau wetu.
“Hivyo ni muhimu kwenu ninyi Wahariri kujua msingi wa mambo muhimu ambayo Taasisi yetu ingependa kuwajulisha viongozi na wananchi kupitia vyombo vya habari” ameongeza Jaji Mwangesi.
Kadhalika, amezungumzia kuharibika kwa Maadili, ambapo amesema sasa hivi suala la Maadili ni kilio kila kona hapa nchini, na kusisitiza kuwa sasa ni jukumu la watu wote kujua namna ya kukabiliana na tatizo hilo na kulitatua.
Kwa upande wake Katibu Idara ya Ukuzaji Maadili Waziri Kipacha akitoa mada kuhusu ukuzaji wa maadili, ameeleza kuwa lipo tatizo la vijana kuingia kwenye mitandao ya kijamii na kuiga mitindo ya maisha ya kigeni na kusahau mila na Desturi za Kitanzania ambazo zinapaswa kuheshimiwa na kulindwa.
“Huku kwetu huwezi kukuta Kijana anabishana na mtu mzima, lakini kwa wenzetu ni vitu vya kawaida, vijana wanaiga mavazi ya ajabu, wanavaa nguo mpaka wewe unayemuangalia unaona aibu, haya yanaingia huku kwa sababu ya utandawazi ambao kwa sasa upo.
“Mbaya zaidi kuna hili ambalo liliibuka hivi karibuni la ndoa za jinsia moja lakini kutokana na weledi wa viongozi wetu wamelikemea, tunaona kama linapungua pungua kidogo, lilitaka kupata msukumo lakini kama nchi tumesimama kidete kuhakikisha tunalinda Maadili”.