• Akaribisha wenye mitaji kuwekeza Tanzania

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema maendeleo ya nchi hayawezi kuletwa na Serikali pekee bali kwa kushirikiana na Sekta binafsi ambayo ni chachu ya kuleta maendeleo kwa wananchi na hivyo Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Dkt. Biteko amesema hayo alipomwakilisha Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Hafla ya utoaji wa Tuzo za Mlaji (Consumer’s Choice Awards Africa) zilizofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 11 Novemba 11, 2023 ambapo viongozi wa Serikali na watendaji wa kampuni mbalimbali walihudhuria akiwemo Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Bi. Latifa Mohamed.

Amesema, “kutolewa kwa tuzo hizi ni kielelezo cha mwendelezo wa jitihada za Serikali katika kuweka mazingira bora ya kibiashara hapa nchini; hivyo wawekezaji wenye mitaji tunawakaribisha mje muwekeze Tanzania na tunawaahidi kwamba Serikali itawapa ushirikiano ili fedha mnazoweka kwenye biashara ziwape faida na pia Tanzania ifaidike kwa uwepo wa miradi husika.”’

Dkt. Biteko amesema Tuzo hizo zilizoanza mwaka 2019 zinahusisha walaji na watumiaji wa bidhaa ambao hutoa maoni na hupiga kura kuchagua kuridhishwa kwao kwa huduma wanazopata kutoka kwa watoa huduma na kueleza kuwa amefurahishwa na namna upigaji wa kura unavyofanyika kwani wale tu wanaotoa huduma bora ndio wanapata nafasi ya kupigiwa kura na kupewa tuzo.

Ameongeza kuwa, kuna kampuni nyingi za kitanzania zinazotoa huduma ndani na nje ya nchi, hususan katika usafirishaji na uuzaji bidhaa hivyo ametoa angalizo kwao kuwa, hilo ni jukwaa kubwa ambalo watoa huduma hao wanaweza kulitumia kwa ajili ya kujitangaza ili huduma na bidhaa zao zijulikane zaidi.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe, Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa, tuzo hizo ni muhimu kwani zinakumbusha umuhimu wa wazalishaji, watoa huduma na wafanyabiashara kumjali yule anayepokea bidhaa yao au huduma yao.

Amesema kuwa, tuzo hizo zimechangia katika uboreshaji wa utoaji wa huduma na bidhaa mbalimbali zinazoenda sokoni hivyo amewapongeza waandaaji wa Tuzo hizo ambazo sasa zimefikia mwaka wa Tano huku wigo wake ukiongezeka kutoka ndani ya Tanzania pekee na sasa ni Afrika kwa ujumla.

Ameeleza kuwa, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lilipitisha itifaki ya biashara ya huduma ndani ya nchi za maendeleo Kusini mwa Afrika hivyo kufanyika kwa tuzo hizo inakumbusha nchi kwamba “tunapoingia katika biashara kwenye eneo huru la biashara Afrika, Tanzania ina jukumu kubwa la kujifunza nini kinatokea duniani, huduma zipi zinatolewa na bidhaa gani zinapelekwa sokoni ili kuweza kutoa huduma ipasavyo kwa viwango vya kimataifa.”

Tuzo za Consumer’s Choice Awards zimeandaliwa na kampuni ya Lavine International Agency na kampuni ya Choice Awards Africa ambapo muanzilishi wa Tuzo hizo ni Bi. Diane Laizer.

Wizara za Nishati Bara, Visiwani zasaini hati ya makubaliano
BAKWATA yakusudia kujenga Zahanati ya Mama na Mtoto