Timu ya Taifa ya Vijana Serengeti Boys chini ya umri wa miaka 17, iliyopo kambini Mjini Rabat nchini Morroco kwa mara nyingine imeishushia kipigo Timu ya Taifa ya Vijana ya Gabon magoli 2-1 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Mjini Rabat.

Aidha, katika mchezo huo Mabao ya Serengeti Boys yamefungwa na, Assad Juma, na la pili kuwekwa kambani na  Abdul Hussein na hicho kinakuwa kipigo cha pili mfululizo kutoka kwa vijana wa Tanzania.

Timu hiyo ya Taifa ya Vijana, Serengeti Boys imeweka kambi ya mwezi mmoja nchini Morocco kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, zinazotarajiwa kuanza Mei 14 hadi 28, mwaka huu nchini Gabon.

Mchezo huo kwa Serengeti Boys unakuwa ni mchezo wa tano wa maandalizi ya fainali za Gabon, baada ya awali kuifunga Burundi mara mbili, kabla ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Ghana Aprili 3 Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo timu hiyo itaendelea kuwa kambini Mjini Rabat hadi Mei 1, mwaka huu itakapokwenda Younde, Cameroon kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya wenyeji Mei 3 na 6, mwaka huu.
Mei 7 timu hiyo itakwenda Gabon ambako imepangwa kundi B pamoja na timu za Mali, Niger na Angola, wakati Kundi A lina timu za wenyeji, Gabon, Guinea, Cameroon na Ghana.

Video: Lissu pasua kichwa, Kumekucha Dodoma
Magazeti ya Tanzania leo Aprili 26, 2017