Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania, Gerald Kusaya amesema Tanzania haitoruhusu kilimo cha bangi hivyo Watanzania wajikite kwenye kulima mazao mengine ya biashara ili kujikwamua kiuchumi.
Taarifa hii inakuja wakati kukiwa na andiko lililosambaa mtandaoni kwamba Tanzania imeruhusu kilimo cha bangi kote Nchini kwa ajili ya matumizi ya dawa.
“Sheria yetu bado iko palepale haijaruhusu kilimo cha bangi na hata Mataifa yaliyoruhusu bangi kulimwa kwa makusudio maalum yakiwemo ya dawa hailimwi kiholela, unaweza kukuta ndani ya hilo shamba la bangi kuna mpaka fensi ya umeme, sasa Watanzania tukiamua kuruhusu huku bangi ilimwe… sasa hivi yenyewe tu hatujaruhusu lakini hali iko hivi, tukiruhusu itakuaje?” amesema Kusaya.
“Kuna namna Watanzania wanaweza kujiogezea vipato kwa kulima lakini sio kulima bangi, mimi nilikua Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo…. Tanzania tuna mazao zaidi ya 100 ya chakula na biashara ambayo Mtu anaweza kupata pesa mfano soya ina soko kubwa, China wanataka tuwapelekee sijui tani ngapi kwa mwezi na bado hatujakidhi hilo soko, Misri wanahitaji mahindi ya njano meli nzima kwa mwezi nani anaweza?” ameongeza Kusaya akiendelea kusisitiza katazo la kilimo cha bangi.