Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa fedha za kujenga kiwanda cha dawa chenye uwezo wa kuzalisha dawa ili kuondoa uhaba wa dawa uliopo na kupunguza bajeti ya dawa zinazonunuliwa kutoka nje ya nchi.
Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee a Watoto Dkt. Godwin Mollel wakati akiongea na kituo kimoja cha runinga nchini.
Dkt Mollel ameeleza kuwa tayari Rais Samia ameshatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha dawa nchini kitachosaidia kuboresha huduma za afya nchini kwa kuongeza upatikanaji wa hali ya dawa na kupunguza matumizi ya fedha ambazo zingetumika kununua dawa nje ya nchi.
“Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha, sasa kinajengwa kiwanda kule Njombe ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha vidonge maana yake ni kwamba bidhaa za Dawa zitashuka bei, dawa ambayo ilikuwa inanunuliwa mara moja itanunuliwa mara mbili mpaka mara tatu,” amesema Dkt. Mollel.
“Kwa kipindi kifupi cha Rais, mama yetu Samia Suluh Hassan alivoingia kwenye Mamlaka, tumepata kiasi cha shilingi Bilion 123 kwaajili ya dawa, hizo ni fedha zilizotoka ndani ya muda mfupi kabla ya hii Bajeti mpya ambayo tumeifanya, ambayo lengo lake ni kwenda kuimarisha suala la Dawa, Vifaa tiba na Vitendanishi,” ameongeza Dkt. Mollel.
Aidha, amekiri kuwa, Serikali imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusiana na dawa, na kueleza kwamba tayari Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima ameshapokea mrejesho kutoka kwa timu ya ukaguzi aliyoichagua kwenda katika hospitali za Mikoa na utekelezaji wake unaanza kufanyiwa kazi ili kudhibiti mianya yote ya upotevu wa dawa nchini.
“Ni kweli kumekuwa na malalamiko mengi kuhusiana na suala la dawa, mmesikia Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gajima ameunda timu zimeenda kwenye hospitali zetu zote za mikoa na wameleta mrejesho, sasa suala la upatikanaji wa dawa sio suala tu la fedha, ukiangalia Serikali imekuwa ikitoa mabilioni ya fedha, mwaka uliopita ilitoa Bilioni 270, ikatoa Bilioni 220 tena, kwahiyo tatizo la upatikanaji wa dawa sio la fedha tu bali uwadilifu na uwazi kwa baadhi ya watoa huduma lakini pia suala la uelewa kwa wananchi,” amesema Dkt Mollel.
Kwa upande mwingine Dkt. Mollel amesema kuwa, Serikali inaendelea kumalizia mchakato wa Bima ya afya kwa wote, utakaosaidia kila mwananchi kuweza kupata huduma bora katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini jambo litakalosaidia kurahisisha matibabu kwa wananchi.