Waziri wa Utamaduni, Sana na Michezo, Balozi Dr. Pindi Chana amesema katika kuendeleza mchezo wa soka hapa Nchini, Serikali inayoongozwa na Rais Samia itamlipa mshahara Kocha wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) Adel Amrouche ambaye ni Raia wa Ubelgiji mwenye asili ya Algeria.
Hayo yamebainishwa leo March 07 2023 wakati wa kumtambulisha Kocha huyo kwenye Ofisi za Wizara zilizopo Mtumba jijini Dodoma ambapo Waziri Dr. Pindi Chana aliambatana na Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Said Othman Yakubu.
Balozi Dr. Pindi Chana amesema Serikali inaamini Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limejiridhisha kuwa ni Kocha Bora atakayekuza soka la Tanzania.
“Ukitazama wasifu wa Kocha Adel utabaini uzoefu mkubwa alionao sio tuu katika kufundisha soka uwanjani, bali pia katika kuandaa Wataalamu wengine wa Soka, hivyo tumtumie vizuri ili asaidie timu yetu kufanya vizuri ndani na nje ya nchi” amesema Balozi Dr. Pindi Chana
Amrouche raia wa Ubelgiji mwenye asili ya Algeria ana uzoefu mkubwa na soka la Afrika baada ya kufundisha klabu na timu za taifa katika ukanda Kusini, Mashariki, Kati na Kaskazini.
Amewahi kuwa Kocha Bora wa Afrika Mashariki mwaka 2013 wakati akiinoa na kuipa Kenya, Harambee Stars ubingwa wa Cecafa Challenge na kabla alifika nusu fainali mara mbili akiwa na Burundi.
Akiwa na Harambee Stars aliweka rekodi ya kucheza michezo 20 bila kupoteza.
Kocha Amrouche amewahi pia kuzinoa timu za taifa za Equatorial Guinea, Botswana, Libya na Yemen kwa nyakati tofauti.
Akiinoa DC Motema Pembe aliiwezesha kufanya vizuri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho akiwa ameipa mara mbili ubingwa wa DR Congo na DRC Super Cup.
Uzoefu mwingine kwa klabu, amezifundisha RC Kouba, USM Alger, alizowahi kuzichezea na MC Algiers, zote za Algeria. Aidha, Kocha Adel ni mkufunzi wa walimu wa Pro Licence wa Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) akizalisha makocha wengi bora barani Afrika na ana uzoefu mkubwa katika soka la vijana, kazi aliyoifanya kwa zaidi ya miaka 10 nchini Algeria na Ubelgiji.
Kocha Amrouche anayezungumza lugha za Kiarabu, Kifaransa, Kingereza na Kiswahili, kwa nyakati tofauti, amewahi kuwa Mkurugenzi wa Ufundi na Michezo katika klabu za Ubelgiji na Ukraine.
Kocha mwenye Uefa Pro Licence na Shahada ya Uzamili katika kuwasoma watu na Utimamu (Mas- ters in Ergonomics in Physical Activity) Amrouche amekuwa akifanya kazi za ukufunzi pia kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) katika kuzalisha walimu wa soka.