Serikali ya Kenya imedhamiria kuwekeza milioni 130 sawa na bilioni 2.2 za kitanzania ili kukiendeleza kilimo cha mirungu kwaajili ya miundombinu ya umwagiliaji na uendelezaji masoko.
Kwa mujibu wa Mtandao wa Taifa Letu umeripoti kuwa Waziri wa Kilimo wa nchi hiyo, Mithika Linturi, fedha hizo ambazo ni sawa na Sh2.2 bilioni za Tanzania, mgao huo utasaidia kuimarisha vyanzo vya maji na uboreshaji wa masoko katika maeneo yanayolima mirungi.
“Pesa hizo zitatumika kujenga mabwawa ili yapatikane maji ya kumwagilia miraa na hivyo kuondokana na kilimo tegemezi kwa mvua.” amesema Waziri Linturi.
Waziri Linturi, ameagiza Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) kushirikiana na Taasisi ya Miraa ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Meru ili kuibua mikakati madhubuti ya kuongeza thamani kwa zao hilo.
“Miraa ilileta pato la Sh6 bilioni mwaka 2022. Serikali imekuwa ikipiga jeki juhudi za uimarishaji wa zao la miraa tangu mwaka 2013 na hadi kufikia sasa, Sh344 milioni zimetumika kuimarisha vibanda vya miraa, vyanzo vya maji na uchimbaji mabwawa. Serikali ya Kenya Kwanza imejitolea kuhakikisha ukuzaji wa miraa unaimarika,” amesema Linturi.
Naye, Mwenyekiti wa Muungano wa Wakulima wa Mirungi Nyambene (Nyamita), Kimathi Munjuri amefurahia hatua ya serikali kutoa fedha hizo kwa sekta ndogo ya kilimo cha mirungi kwa kuwa serikali ilikuwa imesitisha ufadhili mwaka 2020.
Itakumbukwa mwaka 2016, aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Kenya Uhuru Kenyatta alitangaza kutenga dola za Kimarekani 10 milioni kwa ajili ya kusaidia wakulima wa mirungi wakati akitia saini mswada unaotambua mirungi kuwa mmea wa kulizalishia taifa mapato ili uwe sheria.
Pia Rais Kenyatta alitangaza nia ya kuunda jopo kazi la kuangazia changamoto zinazokabili sekta ya ukuzaji wa mirungi ambayo itatoa mapendekezo kwa serikali.