Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanya maboresho ya miundombinu yaliyogharimu zaidi ya Bilioni 6 katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili-Mirembe.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya miradi ujenzi na kuongea na watumishi wa Hospitali hiyo, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema ujenzi huo umefikia hatua za mwisho hivyo itasaidia wananchi kupata huduma za afya katika mazingira bora.
Amesema, “Serikali imetoa zaidi ya Bilioni 6 katika kuboresha miundombinu pamoja na vifaa tiba katika hospitali hii, sasa ni jukumu lenu watumishi kuboresha na kutoa huduma bora kwa wananchi ikiwemo matumizi ya lugha nzuri.”
Aidha, Dkt. Mollel ameiagiza MSD ndani ya miezi miwili kuhakikisha inapeleka vifaa vya upasuaji wa mifupa katika hospitali hiyo ili wananchi waanze kunufaika na huduma hiyo ambayo awali walikua wakiifuata umbali mrefu.
“MSD leteni vifaa vya upasuaji dani ya miezi miwili pia mnatakiwa kutoa kibali cha kununua dawa kwa watu binafsi kwa vituo vyote vya kutolea hhuduma za afya nchini ndani ya saa 24 endapo dawa zinahitajika na hazipo MSD ili kuondoa usumbufu unaoweza kuzuilika kwa wananchi,” amesisitiza.
Hata hivyo, Dkt. Mollel amewashauri viongozi wa hospitali hiyo kuanza kufikiria namna ya kuongeza huduma nyingine ili kutanunua wigo wa kuwahudumia wananchi wenye uhitaji bila kuathiri huduma maalumu za magonjwa ya afya ya Akili zinazotolewa katika Taasisi hiyo.
Kwa upande mwingine Naibu Waziri huyo ameagiza hospitali hiyo kupatiwa gari ya kubebea wagonjwa kutokana na unyeti wa huduma katika hospitali hiyo ili kuokoa maisha ya wananchi wanaohitaji huduma hiyo na kuwaelekeza Wakuu wa Hospitali zote nchini kuacha tabia ya kuwazuia wagonjwa wa rufaa kutoka kituo kingine.
Naye, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Afya Bi. Deodatha Makani amesema wakati hospitali hiyo inaelekea kuwa taasisi ni muhimu watumishi kujipanga na kuwahuduma wananchi kwa ubora wa juu ili kuendana na hadhi ya kuwa taasisi, huku akiweka wazi kwamba Wizara itaendelea kutatua changamoto zote za watumishi.