Timu ya Taifa ya Morocco imejitoa kushiriki Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika CHAN, zilizopangwa kuanza rasmi kesho nchini Algeria.

Morocco imechukua maamuzi hayo baada ya kunyimwa ruhusa ya kusafiri na ndege ya moja kwa moja hadi katika mji wa Constantine, ambako michezo ya nchi hiyo ilipangwa kuchezwa.

Shirikisho la Soka la Kifalme la Morocco (FRMF) limetangaza maamuzi hayo leo Alhamis (Januari 12) kupitia taarifa iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari nchini humo.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa: “Timu yetu ya Soka haiwezi kusafiri hadi Constantine (Algeria), kwa sababu ya ndege ya Royal Air Maroc (RAM) iliyokuwa iwasafirishwe wachezaji na baadhi ya maafisa, kuzuiliwa kufanya safari ya moja kwa moja kutoka Rabat hadi Constantine.”

Desemba 2022, FRMF ilituma Maombi kwa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), ikisisitiza kwamba Morocco haitashiriki michuano hiyo iwapo Algeria itakataa kuuruhusu Msafara wa Morocco kuruka moja kwa moja kutoka Rabat hadi Constantine wakiwa na Shirika rasmi la ndege la Royal Air Maroc.

Ndege ya Shirika la Ndege la Royal Air Maroc

Katika taarifa ya leo, FRMF iimesisitiza kuwa kikosi cha timu ya Taifa ya Morocco kilikua kikiendelea na maandalizi yake kwenye Uwanja wa Mohammed VI kwa kuanzia Januari 6-10, lakini mazoezi hayo yamesitishwa rasmi.

Huku kukiwa na kusitasita na utata wa Algeria, vyombo vya habari vya Algeria vilisisitiza kwamba kutokuwepo kwa jibu rasmi kunaonyesha kukataa kwa Algeria kukubali ombi la Morocco.

Wiki iliyopita, Waziri wa Michezo wa Algeria Abderrazak Sebgag aliapa kwamba nchi yake itawasilisha majibu yake kupitia ombi la Morocco kwa njia rasmi.

“FAF itaijibu CAF kupitia njia rasmi. Algeria ina sheria zake, uhuru wake ambao unazingatiwa juu ya yote,” alisema Waziri Sebgag.

Hata hivyo Chombo cha habari cha Algeria TAS, kilisisitiza kuwa matamshi ya Sebgag “yanaashiria kukataliwa kwa ombi la Morocco.

Mvutano kati ya nchi hizo mbili ulizidi mwaka 2021 baada ya Algeria kuishutumu Morocco kwa kuingilia masuala yake ya ndani.

Utawala wa Algeria pia ulifunga anga yake na kukata uhusiano na Morocco mnamo 2021.
Ikumbukwe kuwa Morocco ndio bingwa Mtetezi wa Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika, wakitwaa ubingwa huo mwaka 2020, nchini Cameroon.

Serikali mbioni kuboresha Hospitali ya Mirembe
Mnzava ataja barabara, maji Korogwe Vijijini