Serikali nchini kupitia Wizara ya Afya, imesema kwa mwaka wa fedha 2022-2023, Serikali ilitenga zaidi ya Milioni 725 kwaajili ya kutekeleza Mpango Mkakati wa tatu wa kitaifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel ameyasema hayo hii leo Juni 7, 2023 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu, Bernabetha Mushashu na kuongeza kuwa pia imeweka mikakati ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kuimarisha ushirikishwaji wa Sekta mtambuka na miundombinu ya utoaji huduma.
Amesema, “katika mwaka wa fedha 2022-2023,Serikali imetenga zaidi ya shilingi milioni 725 kwa ajili ya
kutekeleza Mpango Mkakati wa tatu wa kitaifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza
2021-2026 nchini, huku mikakati mahususi ya udhibiti visababishi vya magonjwa yasiyoambukiza.”
Aidha, Dkt. Mollel amesema Wizara ya Afya pia imeendelea kutoa elimu juu ya njia za kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi, kuzingatia kanuni bora za lishe, kupunguza unywaji wa pombe uliopitiliza na matumizi ya mafuta mengi kwenye vyakula.