Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amekanusha taarifa iliyotolewa na shirika la ndege la Uholanzi (KLM), ya kuwepo kwa hali ya hatari nchini na kusitisha safari zake zilizopangwa kufanyika Dar es Salaam na Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Januari 28, 2023 na Waziri Mbarawa amekanusha taarifa hizo akisema “Taarifa hii haina msingi, haina mashiko, haijali na haina umuhimu na imesababisha hofu isiyo na sababu na kiwewe kwa wananchi na sekta ya anga kwa ujumla. Umma unaaswa kuipuuza hiyo taarifa.”
Amesema, “Wizara inapenda kuufahamisha umma na jumuiya ya kimataifa kuwa, operesheni katika viwanja vya JNIA na KIA zinaendelea. Januari 27, 2023 katika uwanja wa JNIA, ratiba za ndege 17 kati ya 18 zikiwa na abiria 2,545 zimefanuika wakati katika uwanja wa ndege wa KIA, ndege tano zikiwa na abiria 823 zimefanikisha safari zake4”.
Katika taarifa iliyotolewa katika tovuti ya KLM Januari 27, shirika hilo liliwatahadharisha abiria wake na kueleza kusitisha safari katika viwanja vya ndege vya kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA).