Serikali nchini, imeiagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Nchini (LATRA), kupitia Kitengo cha Huduma kwa Wateja kufanya kazi saa 24 ili kutatua kwa wakati changamoto za wasafiri na wasafirishaji.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete jijini Mwanza mara baada kukagua shughuli za udhibiti usafiri wa ardhini na kubaini uwepo wa changamoto mbalimbali ikiwemo utoaji wa vibali vya safari na vibandiko.

Amesema, “Wasafirishaji hawa ni wafanyabiashara akichelewa masaa mawili au matatu tayari amepoteza fedha nyingi na hili ninyi ndio mnasababisha kwa kuchelewesha kuwapa vibali na stika, jipangeni vizuri kuanzia mkoa mpaka makao Makuu ili malalamiko haya yaishe.”

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akizungumza na Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Mkoa wa Mwanza, Bi. Halima Lutavi, wakati alipotembelea Ofisi za Mamlaka hiyo.

Aidha, Mwakibete ameitaka LATRA kukaa na Jeshi la Polisi Nchini ili kufanya kaguzi za kushtukiza na kupanga mikakati inayotekelezeka itakayopunguza ajali nchini kwasababu ajali zimeendelea kuongezeka na kupoteza nguvu kazi ya Taifa katika maeneo mbalimbali nchini.

Awali, Afisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Mwanza, Bi. Halima Lutavi, ameeleza kuwa changamoto ya vibali mfumo unapokuwa na shida LATRA huwasiliana na Jeshi la Polisi ili kuwaruhusu wasafirishaji kuendelea na safari ili kutowachelewesha.

Amesema, kwa sasa Mamlaka inaweka mikakati ya kuboresha usafiri wa pikipiki na bajaji kwa kutengeneza njia maalum ili kuhakikisha kunakuwa na utaratibu mzuri wa usafiri huo katika miji.

Mauaji ya Polisi yaacha simanzi kwa familia
Hans Van Der Pluij: Ninazitaka alama tatu za Young Africans