Serikali imekanusha vikali taarifa zilizotolewa na taasisi isiyo ya kiserikali ya ‘Sikika’ kuwa kuna upungufu mkubwa wa dawa muhimu katika hospitali za Serikali.

Akiongea jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema kuwa taarifa hizo zililenga kuwatia wananchi wasiwasi usio wa lazima.

“Taarifa hizi kwa kiasi kikubwa sio sahihi na sio za kweli, zimetolewa na taasisi moja isiyo ya kiserikali na baadhi ya wanasiasa,” alisema Waziri Ummy.

“Napenda kuwahakikishia wanahabari kwamba suala la afya ni suala la kipaumbele la Serikali hii ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli, na sisi ambao tumepewa dhamana ya kusimamia sekta hii tunao wajibu wakuhakikisha tunavyo vifaa tiba vya kutosha,” aliongeza.

Ingawa alikiri kuwa awali kulikuwa na tatizo la upungufu wa dawa, alisema kuwa tatizo hilo hivi sasa halipo na kwamba Serikali inafanya utaratibu wa kulipa deni inalodaiwa na Bohari ya Dawa (MSD) ikiwa ni katika jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki na bora za afya kwa wakati.

Akizungumzia uwepo wa chanjo katika vituo vya afya na hospitali za umma, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurent Bwanakunu alisema kuwa Bohari hiyo ilipokea chanjo za kutosha wiki iliyopita na kwamba hakuna tena tatizo hilo.

Bwanakunu alizitaka hospitali ambazo bado hazijapata chanjo hizo kufuata taratibu stahiki mapema ili ziweze kuchukua chanjo katika Bohari hiyo ya dawa.

Mahakama Kuu yaridhia CUF kufungua kesi dhidi ya Lipumba, Msajili
Samsung wawataka wateja wao kutupa ‘Galaxy Note 7’, zina tatizo la kulipuka kwenye chaji