Serikali imewahakikishia wananchi kuwa itatekeleza ahadi yake ya kutoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji, ahadi iliyotolewa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama alieleza hayo jana Bungeni wakati akijibu swali la kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani, Freeman Mbowe (Chadema).

Mbowe alihoji ni ’muujiza gani’ ambao serikali itatumia kutekeleza ahadi hiyo itakayogharimu mabilioni ya shilingi wakati  bado kuna changamoto ya utoaji mikopo na upungufu wa dawa hospitalini.

“Namuuliza Waziri, ni miujiza gani itakayotumiwa na Serikali hii ambayo imefilisika, ambayo leo imeshindwa kutoa mikopo ya wanafunzi wa chuo kikuu kwa maelfu, kwamba inaweza kutumia kutafuta fedha hizo shilingi bilioni 960,” alihoji Mbowe.

“Mheshimiwa mwenyekiti nina uthibitisho kwamba jambo hili linatekelezeka. Ni kama tulivyoweza kuwashangaza Watanzania kwa kutoa elimu bure kwa mabilioni ya fedha. Tulivyoweza kuwashangaza Watanzania kwa miradi mikubwa hata ununuaji wa ndege,” Mhagama alijibu.

”Ninaomba kuwathibitishia Watanzania kuwa fedha hizi zitatolewa na wananchi watazipata. Na fedha hizo zitafika hata katika majimbo ya Wapinzani,” aliongeza.

Vikao vya Bunge la 11 vinaendelea mjini Dodoma ambapo miswaada kadhaa ukiwemo Muswada wa Huduma za Habari wa Mwaka 2016 unatarajiwa kuwa sehemu ya mjadala mzito.

Mahakama yamtia hatiani Lady Jay Dee dhidi ya Ruge, Kusaga
Alexis Sanchez Afuata Nyayo Za Messi, Mascherano