Serikali imezindua mpango mkakati wa sekta ya Afya awamu ya tano (HSSP V, 2021-2025) huku ikitarajia kutumia kiasi shilingi trilioni 47 katika kipindi cha miaka mitano kwenye utekelezaji wa mpango huo.
Akizungumza leo Juni 24, 2021 wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dorothy Gwajima amesema mpango huo upo katika maeneo matano ya kimkakati ikiwemo kuboresha utoaji huduma za afya kulingana na mahitaji ambazo ni pamoja na huduma za afya ya mama na mtoto.
Amesema kuwa kila mwaka zitatumika takriban shilingi trilioni 9.4 na kwamba kiasi hicho cha fedha kinatarajiwa kuokoa maisha ya wananchi 200,000 zaidi watakaofikiwa na huduma zilizoboreshwa.
Amesema katika kipindi miaka mitano iliyopita sekta ya afya imepata mafanikio makubwa ikiwemo kujenga vituo vya kutolea huduma za afya 1,887, na katika miaka mitano ijayo Serikali ya awamu ya sita itaendeleza juhudi za kupunguza vifo vya wajawazito na watoto na kuboresha huduma za mama wajawazito.
Aidha, Waziri GWajima ameainisha eneo lingine la kutiliwa mkazo kwenye utekelezaji wa mkakati huo kuwa ni kuimarisha utayari wa kujiandaa kukabiliana na magonjwa ya milipuko na magonjwa ya dharura huku akitolea mfano mlipuko wa covid -19.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo amesema wao kama watunga sera watahakikisha hawaleti vikwazo katika utekelezaji wa mpango huo.