Maafisa wa usalama kaskazini mwa Cameroon, wamefanya mkutano wa dharura kuziomba nchi za Cameroon, Nigeria na Chad kupeleka wanajeshi zaidi katika mpaka wanaoshirikiana, baada ya mashambulizi mapya ya Boko Haran ambayo yameua watu takriban 12 wakiwemo wanajeshi sita siku ya Jumanne.
Maafisa hao, wanasema mamia ya wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu na wenye silaha nzito wamejiingiza katika eneo hilo tete la Ziwa Chad na kushambulia, kupora na kusababisha hofu miongoni mwa jamii.
Maafisa wa Jeshi na serikali katika taifa hilo la Afrika ya kati upande wa kaskazini mwa mpaka na Nigeria, wanasema walifanya mkutano huo wa dharura siku ya Jumatano, chini ya saa 24 baada ya wimbi jipya la mashambulizi ya Boko Haram kuripotiwa.
Hata hivyo, Gavana wa jimbo la Far North nchini Cameroon, Midjiyawa Bakari ambalo linapakana na Chad na Nigeria, alizungumza na kituo cha utangazaji kinachomilikiwa na serikali ya Cameroon CRTV na kusisitiza juu ya hitaji la usalama.