Beki kutoka nchini Ujerumani Shkodran Mustafi amefichua siri ya kukubali kujiunga na klabu ya Arsenal akitokea Hispania alipokua akiitumikia Valencia CF.

Mustafi amefichua siri hiyo akiwa tayari ameshafanyiwa vipimo vya afya huko kaskazini mwa jijini London na sasa anasubiri kutambulishwa kwa waandishi wa habari pamoja na mashabiki wa Arsenal ulimwenguni kote.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 24 amesema kiungo kutoka nchini Ujerumani Mesut Ozil, alikua chagizo kubwa la kumshawishi ajiunge na The Gunners siku chache baada ya klabu hiyo kuonyesha dhamira ya kutaka kumsajili.

Amesema amekua rafiki wa Ozil kwa kipindi kirefu na mara kwa mara wamekua na mazungumzo ya kimaisha, hivyo alipomshawishi afanye hivyo alikubali bila kusita kutokana na kufahamu ukubwa na historia ya klabu ya Arsenal.

“Aliniambia kila kitu kuhusu Arsenal. Ukweli mengi aliyonieleza nilikua nayafahamu kutokana na historia ya klabu hii ambayo muda mwingi nimekua nikiifuatuilia, nilishawishika kwa haraka sana.

“Nilitamani siku moja kuwa sehemu ya kikosi cha Arsenal, Napenda namna wanavyocheza soka, kiuhalisia soka lao halifanani na muonekano wa ushindani wa ligi ya English.

“Soka lao ni kama lile la Hispania pamoja na mfumo unaotumiwa na timu ya taifa ya Ujerumani, kukaa na mpira kwa muda mrefu, hivyo jambo hilo nalo lilichangia kunishawishi.” Alisema Mustafi alipozungumza na Sky Sports

Mustafi amejiunga na Arsenal kufuatia kuumia kwa nahodha na beki wa The Gunners Per Mertesacker ambaye huenda ikiamchukua zaidi ya miezi sita kuwa nje ya uwanja.

“Kwa kipindi kirefu sijabahatika kukutana na Per kwa sababu amestaafu kuichezea timu ya taifa lakini natambua bado ni mchezaji mwenye kiwango cha hali ya juu. Alisema Mustafi

Image result for Shkodran Mustafi with arsenal jerseyShkodran Mustafi

Taarifa za awali zinadai kuwa, Mustafi amekubali kusaini mkataba wa miaka mitano na klabu ya Arsenal, baada ya usajili wake kukamilishwa mwishoni mwa juma lililopita kwa gharama ya Pauni milioni 35.

Mustafi alianza kung’ara akiwa na kikosi cha vijana cha Hamburg ya Ujerumani kabla ya kuhamia nchini England kwenye klabu ya Everton na baada ya hapo alielekea Italia kujiunga na kikosi cha wakubwa cha Sampdoria, na kisha aliuzwa Valencia CF mwaka 2014.

Kwa upande wa timu ya taifa ya Ujerumani, Mustafi amecheza michezo 12 na amebahatika kufunga bao moja katika mchezo dhidi ya Ukraine wakati wa fainali za Euro 2016.

Gazzetta dello Sport Wafichua Mipango Ya Antonio Conte
Cesc Fabregas Aendelea Kukanusha Uvumi Wa Kuihama Chelsea