Tanzania imefungua mpaka kati yake na nchi ya Msumbiji baada ya kufungwa kwa takribani miaka minne, kufuatia kuzorota kwa hali ya usalama na kuibuka kwa wimbi la virusi vya Uviko- 19, hali itakayotoa fursa ya shughuli Mbalimbali za kichumi na kijamii ikiwemo Biashara.
Mkuu wa Wilaya ya Newala iliyopo Mkoani Mtwara, Alh. Mwangi Kundya ameyasema hayo wakatibakifanya mahojiano na kituo cha Habari cha nje ya Nchi TRT na kusema na kudai hatua hiyo ni muhimu na awali wasingeweza kufanya lolote kutokana na hali ilivyokuwa kwa sababu usalama wa raia ni kipaumbele cha kwanza cha Serikali.
Amesema, “hali ya usalama kwa sasa imeimarishwa katika vijiji ambavyo wananchi wa msumbiji walikuwa wanaishi na wakahamishwa na magaidi, sasa wananchi wamesharidhia mpaka kufunguliwa kwa sababu hali ya usalama ni shwari, vikosi vya ulinzi vinaendelea na doria kama kawaida na wananchi wanafanya shughuli zao kama ilivyokuwa hapo awali.”
Kuhusu biashara ya magendo amesema wamedhibiti hali katika mpaka huo wa Mkunya kusini mwa nchi na kuwekwa kwa timu ya maafisa wa Serikali kama Mamlaka ya mapato TRA,kikosi maalum cha polisi pamoja na wataalamu wa mazao ili kuangalia kile kinachongia na kutoka ndani ya nchi.
Waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga Taifa – JKT, Dkt Stergomena Tax kabla ya kufunga mkutano wa Tume ya pamoja ya masuala ya ulinzi na usalama wa tano (JPCDS -5th ) alisema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano kati yake na Msumbiji kwa ajili ya kudumisha amani na usalama kwa raia.
Mbali na kuwahifadhi wapigania uhuru na kuongoza mapambano ya uhuru kusini mwa Afrika, Tanzania na Msumbiji zina uhusiano wa kijamii na kiutamaduni ambapo Msumbiji ni miongoni mwa nchi zisizoweza kuisahau Tanzania kwa mchango wake wa kuhakikisha inapata uhuru Mwaka 1975.