Moto mkubwa umeteketeza bweni la wanafunzi wa shule ya sekondari ya Lowassa iliyoko wilayani Monduli, usiku wa kuamkia jana.

Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu na wanafunzi wa shule hiyo, moto huo ulianza majira ya usiku wakati wanafunzi hao walipokuwa wameenda madarasani kwa ajili ya kujisomea.

Moto huo umeteketeza mali zote zilizokuwa katika jengo hilo ikiwa ni pamoja na vitanda na magodoro; nguo, vitabu na madaftari ya wanafunzi hao.

Mkuu wa shule hiyo, Salim Janitu aliwaambia waandishi wa habari kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme iliyotokea katika jengo hilo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, Izak Joseph na mbunge wa jimbo la Monduli walifika katika eneo hilo la tukio ambapo walianza kufanya jitihada ikiwa ni pamoja na kuomba msaada kutoka kwa wadau mbalimbali na wao kujitolea kiasi cha magodoro na vitu vingine.

“Nimeongea na Mkurugenzi  wa Barrick ameniambia kesho mchana tuonane, nimeongea na Mkurugenzi wa Radio 5, Robert ‘Bob’ Lowassa ameniahidi magodoro 30,” alisema

Mkuu wa Wilaya hiyo, Francis Miti alieleza kuwa kikao cha uongozi kimeamua kuwa wanafunzi hao wapewe mapumziko ya siku saba wakati taratibu nyingine zikiendelea kuchukuliwa.

“Hakuna aliyepoteza maisha. Lakini kwa upande wa miundo mbinu, mnaweza kuona jengo lote limeteketea pamoja na vitu na mali zote zilizokuwa ndani zimetekea,” alisema Mkuu wa Mkoa huyo na kueleza kuwa chanzo halisi cha moto huo kitachunguzwa.

Diamond ampa shavu Idris Sultan
ACT - Wazalendo wairushia rungu CCM, yadai wanataka kusimika utawala wa ‘kiimla’