Leo, ni siku ambayo Rais John Magufuli anatimiza siku 100 tangu alipoanza kazi ya uongozi huo wa ngazi ya juu zaidi nchini huku ripoti na wadau wa maendeleo na wanasiasa wakubwa wakisifia utendaji wake kuwa umetukuka.

Matokeo ya utafiti uliofanywa na timu za watafiti kutoka kampuni mbili za Infotrack Research & Consulting na Medas Touche’ East Africa, Rais Magufuli amepata wastani wa asilimia 84.1 ya alama zilizokuwa zinapima utendaji wake kwa ujumla na namna ambavyo wananchi wa umri tofauti wanavyouchukulia.

Utafiti huo umetumia sampuli ya watu 1200 wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea, kundi ambalo lina watanzania milioni 24.25.

Wanasiasa na wadau mbalimbali wa maendeleo wameonesha kuridhishwa kwa kiwango kikubwa na utendaji wake wa kazi. Miongoni mwao ni waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye ambaye alikihama Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Sumaye alieleza kuridhishwa na utendaji wa Magufuli hususan katika eneo la kupambana na rushwa na ufisadi nchini na kuokoa fedha zilizokuwa zinapotea.

“Lazima tuseme, hakuna haja ya kuficha. Rushwa ilikuwa imejaa kila mahali na ufisadi ulikuwa mchezo wa kila siku. Mimi ningepkuwa Rais ningefanya haya anayoyafanya Rais Magufuli na labda ningefanya zaidi,” Alisema Sumaye katika mahojiano aliyofanya hivi karibuni na gazeti la Mwananchi.

“Nchi ilipofika kulikuwa hakuna namna nyingine ya kuirudisha kwenye mstari bila kuwa na ukali unaoonekana wazi ili wananchi waweze kupata manufaa kutokana na utawala wao,” aliongeza.

Sumaye alieleza kuwa nguvu ya Upinzani mkali wakati wa kampeni ni chanzo cha kile kinachofanywa na Rais Magufuli. Alisema changamoto ile waliyoionesha wakati wa kampeni imeifanya CCM kubadilika huku akiwataka wapinzani kuendelea kuongeza bidii ili kuibana serikali ifanye kazi zaidi.

Mwanamke aliyewanyang’anya Majambazi Bunduki Tarime, aomba azawadiwe Silaha
Dj D- Ommy wa Clouds Fm aachia Mix kali kwa Wapendanao, ‘The Valentine Vol.3 Heart Felt Mixx ", ichukue hapa