Baada ya kufanikiwa kuwazidi nguvu majambazi watatu walivamia kibandani kwake na kumnyang’anya mmoja bunduki aina ya SMG, ameiomba serikali kumpa silaha ili ajilinde.

Sophia Manguye ambaye ni mkazi wa kijiji cha Buriba, kata ya Sirari wilayani Tarime mkoani mara, mwenye umri wa miaka 46, amesema kuwa baada ya tukio hilo ameanza kupata vitisho kutoka kwa watu mbalimbali na kadri habari zinavyozidi kusambaa ndivyo anavyoingia hatarini zaidi.

“Ingawa Mungu ndiye aliyenilinda, lakini ninaomba serikali inipe silaha kwa ajili ya ulinzi wangu na familia yangu, kwani hawa watu wanaweza kurudi na kunimaliza kwa sababu nimesababisha wamepoteza bunduki yao,” alisema Manguye.

Watu hao watatu wanaosadikika kuwa ni majambazi, walivamia katika kijiji hicho mwanzo mwa wiki hii na kuanza kupora pesa na vocha za simu kwenye maduka mbalimbali, lakini walipofika kwenye duka la Bi. Manguye alifanikiwa kumkamata mwenye silaha na kung’angania huku akipiga kelele.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, Gemini Mushi, ingawa Bi. Manguye alipata majeraha wakati wa purukushani hiyo, hakumuachia jambazi huyo hadi pale ambapo polisi na wananchi walipofika na kumtia mbaroni huku wenzake wawili wakifanikiwa kutimua mbio.

Maalim Seif ailima ZEC barua
Siku 100 za Magufuli: Sumaye amwagia sifa, Tafiti zaonesha anavyokubalika