Mwenyekiti wa Kituo cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali na Taarifa MECIRA, Habibu Mchange amesema kuwa shughuli za kibinadamu zinazofanywa na wananchi wachache katika bonde la Ihefu ndio wamekuwa chanzo cha kukauka kwa Mto Ruaha.
Amesema hayo, katika Kongamano la Wahariri na Wadau wa Uhifadhi, Mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji hii leo Decemba 19, 2022 Mkoani Iringa, ambapo ameeleza kuwa takribani siku 130 mto Ruaha mkuu (Great Ruaha) haujatiririsha maji kutokana na uharibifu wa bonde la Ihefu unaofanywa na baadhi ya wananchi kwa ajili ya maslahi yao binafsi.
Mchange amesema, kutokana na uharibifu huo kumepekea wanyama wengi katika hifadhi ya Taifa Ruaha kufa na wengine kuambukizwa magonjwa mbalimbali kutokana na kukosa maji ya kutosha.
Ameongeza kuwa, serikali inatakiwa kuchukua hatua kali kwa wananchi wote ambao wamekuwa wakiharibu mazingira ili kunusuru wanyama waliopo katika hifadhi ya Taifa Ruaha
Aidha, ameeleza kuwa zaidi ya asilimia 60 ya ardhi ya Tanzania imeharibika na asilimia 16 ya nchi ya Tanzania ni Jangwa kutoka na uharibifu wa kimazingira unaofanywa na baadhi ya wananchi.
“Mto Ruaha na mito mingine kama hatua za haraka hazitachukulia basi tutavuna mabua kutokana na uharibifu unaoendelea,” Amesema Mchange.
Mchange aongeza kuwa zaidi ya hekari laki nne za misitu zimeharibiwa na baadhi ya wananchi wasiokuwa na mapenzi ya nchi yao hivyo serikali inatakiwa kuchukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo.
Amemalizia kwa kusema kuwa waandishi wa habari wapo tayari kuisaidia serikali kuibua na kuandika habari za kuelimisha na kuwafichua waharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji.