Baada ya kufanikiwa kutinga Nusu Fainali ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrikakwa Wanawake inayoendelea nchini Morocco, Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Barbara Gonzalez, amesema Uongozi unakiamini kikosi hicho na wanachotakiwa ni kuendelea kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Simba Queens itacheza Mchezo wa Nusu Fainali dhidi ya Mabingwa watetezi, Mamelodi Sundowns Queens kutoka Afrika Kusini ambayo jana Jumapili (Novemba 06) usiku, ilipambana na TP Mazembe Queens kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Barbara amesema wachezaji wanatakiwa kucheza kwa bidii katika Mchezo huo wa Nusu Fainali na Uongozi unaamini timu hiyo itaweza kupata matokeo mazuri na kutinga Fainali.
“Napenda kuwaambia klabu ilipanga kuwapa Sh. milioni 100 kama bonasi naimefanya hivyo kwa sababu wachezaji wetu walishinda mchezo dhidi ya Green Buffeloes, ninajua klabu ina mambo mengi, lakini kwa sasa tumeweka nguvu na akili katika upande huu ili kuhakikisha tunashinda kila mchezo ulio mbele yetu,” amesema Barbara.
Mbali na Bonas hiyo kwa wachezaji, Simba Queens imejihakikishia kitita cha Dola za Marekani 200,000 (sawa na Sh. milioni 465.4 zinazotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kufautia kutinga hatua ya Nusu Fainali.
Mbali na zawadi hiyo ya Nusu Fainali, Bingwa atajinyakulia kitita cha Dola za Marekani 400,000 sawa na Sh. milioni 930.9, wakati mshindi wa pili atajinyakulia zawadi ya Dola za Marekani 250,000 ambazo ni sawa na Sh. milioni 581.8.