Klabu ya Simba imezindua Jezi mpya za klabu hiyo zitakazoanza kutumia kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea Visiwani Zanzibar.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Simba SC Ahmed Ally amesema Jezi hizo ni maalum kwa michuano hiyo sambamba na ile ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, ambapo klabu hiyo itacheza hatua ya makundi kuanzia mwezi Februari.

Ahmed amesema Jezi hizo pia zitavaliwa na mashabiki wa Simba SC na kuanzia sasa wanaweza kuzipata nchini kote.

“Tumezindua Jezi mpya ambazo tutaanza kuzitumia kwenye michuano ya Mapinduzi hapa Zanzibar, pia tutazitumia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.”

“Mashabiki wanaweza kununua Jezi mpya kwa ajili ya klabu yao, imekua ni kawaida yetu kufanya jambo hili na wengine wamekua wakituiga.” amesema Ahmed Ally.

Simba SC iliyoondoka Dar es salaam majira ya asubuhi, itaanza mchakato wa kulisaka taji la Mapinduzi 2022, keshokutwa Jumatano (Januari 05), kwa kucheza dhidi ya Selem View Uwanja wa Aman.

Simba SC imeelekea Zanzibar ikiwa na kikosi chake kamili, huku Kiungo Mshambuliaji kutoka Malawi Peter Banda akiwa kwenye majukumu ya timu yake ya taifa The Flames inayojiandaa na Fainali za Mataifa ya Afrika 2022 zitakazounguruma nchini Cameroon kuanzia mwishoni mwa juma hili (Januari 09).

Mwaka 2021 Simba SC ilifika Fainali ya Kombe la Mapinduzi na kupoteza kwa changamoto ya Mikwaju ya Penati dhidi ya Young Africans.

Polisi Afrika Kusini inamshikilia mtu mmoja anayehusishwa na Moto uliounguza Bunge.
Rais Mwinyi atengua uteuzi wa Mkurugenzi ZBC