Uongozi wa klabu ya Simba SC umekanusha taarifa za kumfukuza kazi kocha Joseph Omog, kama ilivyoripotiwa katika mitandao ya kijamii mapema hii leo.
Kwa niaba ya uongozi wa klabu ya Simba, mkuu wa idara ya habari na mawasilino wa klabu hiyo ya Msimbazi Haji Manara amezungumza na Dar24 na kusema, Simba haijatoa taarifa yeyote kuhusiana na mabadiliko yanayoenezwa kwenye mitandao ya kijamii.
Manara amesema anaamini wanaotoa taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii hawaitakii mema klabu ya Simba, ambayo bado inamuamini kocha huyo kutoka nchini Cameroon.
‘Nimeshaeleza toka awali kuwa, hakuna mechi tano wala huo mpango wa kumwondoa kocha Omog au benchi zima la ufundi, klabu ya Simba haina mpango huo.
‘Tunaomba mashabiki, wapenzi na wanachama wa klabu ya Simba kuweka Imani yao kwa Uongozi, kikosi cha Simba na benchi la ufundi kuwa tunajua nini mashabiki wetu wanachotaka na ndicho tunachopambana kuhakikisha tunafikia malengo’ alisema Haji Manara alipoongea na Simba News kuhusiana na ujumbe unaosambazwa wa kuvunjwa kwa benchi la ufundi la Simba.
Manara ameongeza kuwa, klabu ya Simba itaendelea kuhakikisha inatoa taarifa sahihi na kwa wakati kupitia njia zake za mawasiliano chini ya Mkuu wa idara yake ya Habari na Mawasiliano na sio kwingineko.
Wakati huo huo kikosi cha Simba kimerejea jijini Mwanza kutokea Tabora ambako kilicheza mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya timu ya Milambo.
Kikosi cha Simba kimeweka kambi jijini humo kwa ajili ya maandali ya mchezo wake dhidi ya Stand United siku ya Jumapili tarehe 01.10.2017